MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, June 24, 2009

CUF yaanza kuweweseka kwa Lwakatare

Salim Said
SIKU chache baada ya Willfred Lwakatare kuvua nyadhifa zake zote na kurudi jimboni kwake, CUF imeanza kudhibiti nyendo zake baada ya kumzuia kufanya mikutano ya hadhara.


Mkurugenzi wa habari na uenezi wa CUF, Ashura Mustafa aliiambia Mwananchi jana kuwa chama hicho kimesambaza barua katika wilaya na matawi yake yote nchini kuwaagiza watendaji wake wamdhibiti Lwakatare ili asifanye mikutano kwa mgongo wa chama.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Lwakatare, ambaye amekuwa akiripotiwa kuhutubia mikutano ya hadhara akiuliza watu ahamie chama gani, haruhusiwi kufanya mkutano wowote isipokuwa kwa idhini ya makao makuu.

Nafasi ya Lwakatare, ambaye aliondolewa katika kutetea nafasi yake ya naibu katibu mkuu baada ya kuuishikilia kwa karibu miaka 10, ilichukuliwa na Joram Bashange. Kwa upande wa Zanzibar, nafasi hiyo inashikiliwa na Juma Duni Haji.

Kitendo hicho kilimfanya aandike barua ya kujivua nyadhifa zote kwenye chama hicho na kubaki na mwanachama wa kawaida.

Jana Ashura aliliambia gazeti hili kuwa pamoja na chama kusambaza barua hizo za kumzuia Lwakatare kufanya mikutano, pia kinakusudia kutoa tamko zito dhidi ya mbunge huyo wa zamani wa Bukoba Mjini.

Alisema anachofanya Lwakatare si kuimarisha chama kama alivyodai kwenye barua yake kwa mwenyekiti alipotaka kujiuluzu bali kukivuruga katika kipindi hiki cha kukaribia chaguzi za kitaifa.

“Ni kweli tumewaandikia wenyeviti wa chama katika kata na wilaya zote Tanzania Bara na hasa Kanda ya Ziwa kuwataka kuwataka wamzuie Lwakatare kufanya mikutano ya kukivuruga chama kwa kuwalisha sumu wa wananchi akitumia jina la CUF,” alisema Mustafa.

“Tumewaagiza kama atataka kufanya mkutano wowote kwa jina la CUF asiruhusiwe, badala yake waripoti makao makuu, halafu tutaangalia lengo la mkutano huo. Tukijiridhika tunaweza kuruhusu lakini bila hivyo asifanye.”

Alisema Lwakatare sasa hana mamlaka kikatiba kufanya mkutano wowote kwa jina la CUF kwa sababu si kiongozi tena wa chama bali mwanachama wa kawaida.

“Kwa vile ameamua kujivua nyadhifa zake zote ndani ya chama na chama kimeridhia, hana tena mamlaka ya kuitisha mikutano ya wanachama; uwe wa hadhara au wa ndani,” alisema Mustafa.

Mwishoni mwa wiki iliyopita mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alimsihi Lwakatare kutoharibu chama baada ya kujiengua katika nyadhifa zake.

Habari za ndani zinasema kuwa tayari viongozi wakuu wa chama hicho- Prof Lipumba, katibu mkuu Seif Sharif Hamad na makamu mwenyekiti Machano Khamis- wamekutana kujadili namna ya kukihami chama na kile kilichoelezwa kuwa mkakati wa Lwakatare kutaka kukichafua.

Inadaiwa kuwa katika kikao hicho, Machano, ambaye alifanya ziara fupi Kanda ya Ziwa baada ya Lwakatare kujiuzulu, alieleza mambo aliyoyaona wilayani Bukoba kuhusu maendeleo ya chama chao.

Akizungumzia uamuzi huo wa CYF, Lwakatare aliiambia Mwananchi kuwa hana taarifa ya agizo hilo kwa kuwa anaamini halijafika wilayani kwake Bukoba mjini.

“Huku hili agizo au barua halijafika na ikifika tutaijadili kuona kitu gani cha kufanya kuweza kufanya kazi yangu ya kuimarisha chama,” alisema Lwakatare jana.

“Mimi bado ni mwanachama wa CUF na nilisema kwamba uamuzi wa kujiunga na chama chochote upo mikononi mwa familia yangu, wananchi na viongozi wangu wa CUF,” alisema Lwakatare alipozungumza kwa njia ya simu akiwa Bukoba.

No comments:

Post a Comment