MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Thursday, June 25, 2009

Chadema kumpokea Lwakatare Bukoba Mjini leo

Salim Said
ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Tanzania Bara Wilfred Lwakatare, ametangaza rasmi kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na leo anatarajiwa kupokelewa rasmi na wanachama wa chama hicho mjini Bukoba.


Baada ya kupokelewa leo, kesho Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe atampa kadi chama hicho katika hafla maalumu, itakayofanyika katika Jimbo la Biharamulo Magharibi, kabla ya kuanza kupanda majukwani kumnadi mgombea wa chama hicho katika kinyang'anyiro cha ubunge.

Lwakatare ambaye alishika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara kwa zaidi ya miaka 10, alitangaza hayo jana baada ya kupata ushauri kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki zake.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu akiwa wilayani Bukoba, Lwakatare alisema:“Mimi ni Chadema kuanzia jana (juzi) saa 1:30 usiku, nyinyi mko nyuma sana kwa sababu taarifa hizi zimefika Ujerumani nyinyi Dar es Salam hamjapata!”

Lwakatare alitangaza kujiondoa CUF kupitia mahojiano yake ya moja kwa moja na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani juzi saa 1:30 usiku.

Alisema uamuzi huo aliuchukua baada ya kufanya kikao na familia yake, mzazi wake na wanachama wake 284, na kuwaeleza mkasa uliomfika, wanachama 282 walimwambia aende Chadema na kwamba wanachama wawili tu walimtaka aende Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Mzazi wangu ameniambia niende Chadema, familia pia imeniambia hivyo hivyo wanachama 282 katika kikao waliniambia ‘nenda chadema’ isipokuwa wawili walioniambia ‘nenda CCM’ kwa hiyo wengi wameshinda,” alisema Lwakatare.


Pamoja na uamuzi huo, Lwakatare aliwataka viongozi wa CUF kujifunza kwa kupitia vitabu yake kuanzia namba moja hadi tatu ambavyo amewatumia ili kurekebisha chama chao kwa kuwa si chama chake.

Alisema bado anaamini kuwa ukombozi wa Watanzania ni vyama vyote kuungana ili kujenga nguvu moja ya mapambano na CCM, na kwamba bila hivyo CCM itaendelea kutawala nchini.

“Licha ya kujiunga na Chadema niko tayari kushirikiana na CUF kwa lengo la kuunganisha nguvu ya upinzani kuing’oa CCM,” alisisitiza Lwakatare.

Naye Mwenyekiti wa CUF taifa Profesa Ibrahim Lipumba alisema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa kwa kuwa Lwakatare alikuwa mjumbe katika Baraza Kuu la Uongozi la chama na mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa.

“Tunasikitika sana kwa sababu alikuwa kiongozi wetu na tulikuwa naye muda mrefu. Tulifanya mabadiliko ili kumpa muda wa kuimarisha chama lakini ameamua kufanya uamuzi huo, tunasikitika sana.

“Licha ya jitihada zangu za kuzungumza naye sana na kumsihi ameamua hivyo, mimi nilidhani tumeshaelewana na kuyamaliza kumbe ilikuwa bado. Lakini kukosa unaibu si sababu ya kuhama chama,” alisema Profesa Lipumba.

Lwakatare aliwahi kuwa mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini na Mwenyekiti wa Kambi ya upinzani Bungeni kupitia tiketi ya CUF na hatimaye sasa ameamu kujiunga na Chadema baada ya kuangushwa Machi mwaka huu katika nafasi yake ya unaibu Katibu Mkuu.

Wakati huohuo, aliyekuwa naibu katika mkuu wa chama cha wananchi CUF Alfred Rwakatare kesho anatarajia kujiunga rasmi na chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema na kukabidhiwa kadi ya uanachama na mwenyekiti wa taifa wa chama hicho Freeman Mbowe.

Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi wa oparesheni na uchaguzi wa Chadema John Mrema alisema kuwa Rwakatare ataingia rasmi Chadema ijumaa na kukabidhi kadi ya uanachama katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanjwa wa Uhuru mjini Bukoba.

Mrema alisema mara baada ya Kukabidhiwa kadi hiyo na kuwa mwanachama rasmi Rwakatare atawasili jumamosi Biharaulo magharibi kwa ajili kusaidia kampeni za kumnadi mgombea wa chadema Dk. Grevas Mbassa pamoja na viopngozi wengine wa Chadema.

Aliwataja viongozi hao kuwa ni pamoja na Dk. slaa, Philimoni Ndesambulo pamoja na Zitto Kabwe ambao baada ya zoezi hilo nao pia wataingia Biharamulo kwa ajili ya kusaidia kampeni za chama chao.

No comments:

Post a Comment