Salim Said
KAMPENI za uchaguzi wa Baraza Kuu la Waislaam Tanzania (Bakwata) katika ngazi ya Wilaya zinaendelea, huku ishara za kutokea kwa vurugu za hapa na pale zikianza kuonekana mapema.
Baadhi ya wagombea wamewashutumu wengine kuwa, wanatoa vitisho kwa lengo la kudhoofisha nguvu zao katika kampeni hizo ambazo zinatarajiwa kuishia mwishoni mwa mwezi huu.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, mgombea mwenyekiti wa Bakwata Wilaya ya Temeke sheikh Ali Mtulya alidai, amekuwa akitumiwa ujumbe wa vitisho kupitia simu yake ya mkononi mara kwa mara.
Alisema, wanaomtumia ujumbe huo hawajui na kila anapojaribu kupiga namba zinazotumiwa kutuma ujumbe huo, huwa hazipatikani.
“Haya hayaashirii mema katika uchaguzi huu, nimekuwa nikitumiwa meseji za vitisho na matusi kupitia simu yangu ya mkononi na kila nikijaribu kupiga simu hizo hazipatikani,” alisema sheikh Mtulya.
Sheikh Mtulya, ambaye anatetea nafasi yake ya Mwenyekiti wa Wilaya hiyo, alimshutumu sheikh Mkuu wa Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum kuwa, amekusudia kuandaa watu kwa ajili ya kumng’oa.
Alidai, katika hotuba ya uzinduzi wa msikiti wa Bakwata Wilaya hiyo sheikh Salum alisema kuwa, atahakikisha sheikh Mtulya haingii madarakani.
“Sheikh wa Mkoa katika hotuba yake ya uzinduzi wa msikiti wa Bakwata Wilaya ya Temeke alisema kwamba, atahakikisha mimi sirudi madarakani na ataandaa watu wake kuhakikisha anatimiza azma hiyo,” alisema Sheikh Mtulya na kuongeza:
“Yeye kama sheikh wa mkoa alitakiwa kutoa hotuba nzuri ya kuhamasisha amani na utulivu katika uchaguzi wetu, badala ya kuharibu. Eti kwa sababu mimi sikumpigia kura alipogombea usheikh wa mkoa na ni kweli sikumpigia.”
Alisema, kutoka na kauli hiyo wanaandaa tamko la kulaani kauli ya sheikh Salum na baadaye wataliwasilisha Bakwata Makao Makuu.
Kwa upande wake sheikh Salum ambaye ni sheikh wa mkoa wa Dar es Salam alikiri kusema maneno hayo, lakini alidai kuwa alizungumza maneno hayo kwa utani tu na wala hayakuwa na ukweli wowote.
“Mimi yule ni shemegi yangu ametuolea, kwa hiyo mimi nilisema kama kumtania tu, kwa sababu mtu akitaka kufanya ubaya kwa mwengine hasemi bali hufanya kimya kimya,” alisema Sheikh Salum.
Alisema, kama wao wameyachukulia kweli ni upuuzi, kwa kuwa kama anataka kumfanyia ubaya hana haja ya kuandaa vijana bali angesubiri majina ya wagombea yatakapofikishwa ofisini kwake na kuliondoa jina lake.
“Lakini mimi sina ubaya na mtu yoyote, wote nimewasamehe,” alisema sheikh Salum.
Alisema, kama kuna watu wamejitokeza kupambana na sheikh Mtulya kwa kuchukua fomu wanatumia haki yao ya kidemokrasia na hawakuandaliwa na yeye.
“Kama kuna vijana wamechukua fomu, wanatumia demokrasia yao, lakini sijawandaa mimi. Na kama wanaandika tamko la kulaani ili waliwasilishe Bakwata makao makuu ni upuuzi tu,” alibeza sheikh Salum.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Bakwata ustadh Issa Mkalinga, alithibitisha kupata malalamiko hayo kutoka kwa Sheikh Mtulia na kwamba uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Juni 28 kwenye shule ya Sekondari ya Thaqafa Tandika jijini hapa.
Alisema, tayari wamemaliza chaguzi katika ngazi ya Msikiti na Kata kwa kiwango kikubwa nchini na kwamba sasa wanaingia katika ngazi ya Wilaya halafu Mkoa na kumalizia na Taifa.
No comments:
Post a Comment