MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, June 17, 2009

Mkulo: Pato la taifa litaanguka hadi 2011

Salim Said
WAKATI ukuaji wa uchumi katika mataifa ya Ulaya na Marekani ni wa kukimbia, ule wa nchi za Afrika unazidi kudorora kwa kurudi nyuma hatua kadhaa badala ya kusonga mbele.

Haya yanathibitishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi Mustapha Mkulo katika ripoti yake ya kurasa 26, kuhusu ‘Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2008 na Malengo ya Uchumi Katika Kipindi cha Muda wa Kati (2009/2010 hadi 2011/2012)’.

Waziri Mkulo anathibitisha katika ripoti hiyo, kuanguka kwa pato la taifa kulikosababishwa na kuyumba na kutikisika kwa uchumi wa dunia kuanzia Marekani, Ulaya hadi Afrika.


Awali, kabla ya Mkulo kukiri kuanguka kwa uchumi wa taifa, wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kiuchumi, walidokeza anguko hilo wakiwamo, Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini Esther Mkwizu.

Wachambuzi hao walisema, mtikisiko wa kiuchumi unaoendelea kuikumba dunia una sura ya herufi ‘L’ ikiwa na maana kwamba, uchumi utaanguka hadi chini na utakaa kwa muda wa miaka mitatu hadi mitano ndipo utanyanyuka na kutengamaa.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, hiyo inasababishwa na benki na kampuni kubwa za kimataifa kuanza kufilisika, huku shughuli za kiuchumi zikizidi kuanguka licha ya benki hizo, kushusha riba hadi asilimia 0.0.

Maneno haya ya profesa Lipumba na Mkwizu yanathibitishwa na waziri Mkulo kwa kusema, pato la taifa kwa mwaka 2009 litaanguka kwa asilimia 2.4 ambapo ukuaji wake utakuwa ni asilimia 5.0 ikilinganishwa na asilimia 7.4 mwaka 2008 na asilimia 7.1 mwaka 2007.

Mkulo anasema, ukuaji huo wa pato la taifa mwaka 2008, ulichangiwa zaidi na kuongezeka kwa viwango vya ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika sekta ya kilimo, uvuvi na huduma.

Anasema, ukuaji wa viwango vya juu vya pato la taifa mwaka 2008 ulijionesha katika shughuli ndogo ndogo za kiuchumi za mawasiliano asilimia 20.5, fedha 11.9 na ujenzi asilimia 10.5.

“Hata hivyo kiwango cha ukuaji katika shughuli za kiuchumi za viwanda na ujenzi kilipungua kidogo ikilinganishwa na mwaka juzi,” anasema Mkulo.

Kwa mujibu wa Mkulo, pato la taifa si tu kuwa litaanguka kwa mwaka 2009, bali litaendelea kudorora katika kipindi chote cha muda wa kati ambapo mwaka 2010 ukuaji ni asilimia 5.7 na kwamba pato hilo litatengamaa mwaka 2011/2012 kwa kufikia kiwango cha asilimia 7.5.

“Ili kukabiliana na hali hiyo, serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kukuza pato la taifa na kupunguza umasikini na kwa kuzingatia hilo hatua zinachukuliwa kuboresha mazingira ya kuziwezesha sekta hizo kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi,” anasema Mkulo.

Anasema, serikali ina mpango wa kukamilisha sera ya ubia kati ya sekta ya Umma na Binafsi (PPP Policy) ili kuharakisha maendeleo ya sekta binafsi na kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini nchini.

Anasema, pia serikali itaongeza ufanisi katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma, biashara, kilimo, uwekezaji na kupunguza matumizi ya serikali yasiyo ya lazima katika mapato yake.

Mkulo ansema, serikali kwa kuzingatia chanzo cha mtikisiko huo, Benki Kuu (BoT) imeanzisha utaratibu wa uangalizi na usimamizi wa taasisi za fedha kila siku, ili kubaini matatizo yatakayojitokeza na kuchukua hatua za haraka.

“Kwa kupunguza makali na kuhimili shinikizo la mtikisiko huo hususan katika kuwalinda wananchi walio kwenye hatari kubwa zaidi, Serikali inalinda ajira, hasa katika shughuli zitakazokumbwa na ukwasi kutokana na kupungua kwa utashi wa bidhaa na huduma wanazotoa,” anasema Mkulo.

Anasisitiza, ili kuinusuru nchi kutokana na athari za kuadimika kwa chakula, serikali inaongeza kasi katika kilimo, kulinda programu muhimu za kijamii na uwekezaji kwa maendeleo ya nchi.

Huku pato la taifa likiporomoka kwa asilimia 2.4 kwa mwaka 2009, nchi inakabiliwa na matatizo ya mfumko wa bei, kushuka kwa thamani ya sarafu mambo ambayo, serikali inasema haina uwezo wa kuyadhibiti kwa madai kuwa ni ya kimfumo na yanategemea zaidi nguvu ya uchumi wa soko.


Waziri Mkulo, anasema tatizo la kushuka kwa thamani ya sarafu halizuiliki kwa sababu ni la kimfumo na linasababishwa na mfumuko wa bei za bidhaa muhimu na upatikanaji wa fedha za kigeni, ambao ni wa msimu. “Mheshimiwa Mwenyekiti tutake tusitake, tatizo la kupanda na kushuka kwa sarafu ya Tanzania lipo na serikali haiwezi kulizuia kwa sababu ni la kimfumo,” anasema Mkulo.

Anafafanua, kinachofanywa na serikali kukabiliana na tatizo hilo ni kuangalia iwapo mzunguko wa shilingi ya Tanzania unaendana na uchumi wa soko au vinginevyo.

“Kama mzunguko ni mbaya tunaweza kuingilia na kurekebisha lakini, kama unaendana na uchumi wa soko, hatuwezi kuingilia hata kidogo,” anasisitiza Mkulo.

Mkulo anathibitisha, “Upatikanaji wa fedha za kigeni nchini kuwa ni wa msimu hususan wa mavuno kuanzia Juni hadi Disemba ya kila mwaka, lakini pia tukiweza kudhibiti mfumko wa bei za bidhaa muhimu tunaweza kudhibiti thamani ya Shilingi yetu.”

Kwa mujibu wa Mkulo, thamani ya Shilingi ya Tanzania imeshuka hadi kufikia wastani wa Sh280.30 kwa Dola ya Marekani Desemba mwaka jana ikilinganishwa na Sh1,132.09 Desemba 2007.
Anasema, mfumko wa bei kwa mwaka 2008, ulikua kwa asilimia 10.3 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2007, ambapo kiwango cha chini cha kasi ya mfumko huo 2008, ilikuwa Januari kilipopanda kwa asilimia 8.6 na kiwango cha juu asilimia 13.5 Disemba mwaka huohuo. “Lengo letu la ukuaji wa mfumko lilikuwa asilimia 5.0 Juni 2008, lakini halikufikiwa kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji hasa baada ya kupanda kwa bei ya nishati hususan mafuta na umeme,” anasema Mkulo na kuongeza:

“Hadi April 2009, mfumko ulifikia asilimia 12.0 kutokana na hali hiyo, ambapo awali lengo la mfumko huo lilitarajiwa liwe chini ya asilimia 7.5 ifikapo Juni 2009, lakini sasa tunatarajia asilimia 11.0 ya mfumko.”

Mkulo anasema, ili kuhakikisha wanarudisha utengamano wa pato la taifa serikali itakabiliana na mtikisiko wa uchumi duniani, kuongeza uwekezaji katika maeneo ya mwingiliano wa kisekta hususan kilimo, miundombinu, uzalishaji viwandani na nishati ikiwa ni pamoja na kuhimiza ushirika wa sekta binafsi katika maeneo hayo.

“Serikali itaongeza upatikanaji wa mikopo hasa kwa sekta ya kilimo kwa kuwa na benki ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula,” anasema Mkulo.

Anasema, serikali itaongeza na kuboresha mapato ya ndani ili kugharamia sehemu kubwa ya matumizi ya serikali, kuimarisha usimamizi katika matumizi ya fedha za umma na kuendelea kulinda mafanikio yaliyopatikana.

“Serikali itaendelea kulinda na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta za kijamii na kuboresha utoaji wa huduma ili kuongeza wigo wa ukusanyaji na ukuzaji wa pato la taifa,” anasema.

Anasema, serikali pia itaongeza na kuboresha mipango ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kuongeza ajira pamoja na kupima ardhi ya vijijini ili wamiliki waweze kutumia hati zao kupatia mikopo.

No comments:

Post a Comment