MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, June 17, 2009

TGNP waisifu bajeti ya Serikali

Salim Said
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeisifia bajeti ya serikali ya mwaka 2009/10 kwa kuwa imelenga kukuza pato la ndani na kupunguza utegemezi kwa wahisani na misaada ya nje.


Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao huo, Usu Mallya katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyoandaliwa na timu ya wataalamu wa jinsia na maendeleo katika semina ya wiki moja.

Mallya alisema, bajeti hiyo imewekeza fedha nyingi katika sekta mmuhimu za kijamii na kiuchumi zikiwamo za elimu, kilimo, miundombinu na maji.

“Tumefurahishwa sana na bajeti ya mwaka kwa kutenga fedha nyingi katika vipaumbele muhimu vya kijamii na kiuchumi, japokuwa kuna ukosefu wa taarifa za kuhakikisha fedha hizo zinawafaidisha walengwa,” alisema Mallya na kuongeza:

“Hususan makundi ya watu yanayotengwa na kukandamizwa kimaendeleo ambao ni pamoja na wanawake, waathirika wa virusi vya ukimwi na watu wenye ulemavu.”

Alisema wanakubaliana na mpango wa serikali wa kupunguza matumizi ya fedha za umma kwa katika gharama za safari, semina, makongamano na ununuzi wa magari ya kifahari.

“Japokuwa hii si mara ya kwanza kwa serikali kupitisha maamuzi kama haya, lakini swali la kujiulza hapa ni vipio kuhusu ukubwa wa serikali kuu yenye mawaziri 26,” alisema Mallya.

Alisema, TGNP inaunga mkono juhudi za serikali katika kujinasua na athari za mtikisiko wa kiuchumi duniani, kwa kuongeza uzalishaji wa chakula cha ziada na kuimarisha miundombinu na mawasiliano ili kuweza kuhimili ushindani wa soko la kikanda na kidunia.

“Ni ulinzi wa aina gani ambao serikali imeuweka katika kulinda ajira za watanzania, soko la mazao ya Tanzania na viwanda vidogo na vya kati ambavyo vimeathirika mitaji yao kutokana na mtikisiko wa kiuchumi,” alihoji Mallya.

Alisema, serikali za magharibi zilibaini athari za mitikisiko huo mapema na kuanza kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na hali hiyo katika sekta za uchumi na fedha.

Hata hivyo Mallya alisema, fedha nyingi zinahitajika ili kufikia malengo ya milenia ya usawa wa kijinsia kwa asilimia 50 kwa 50 kati ya wanaume na wanawake, katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Aliitaka serikali kuimarisha wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuongeza kodi kwa makampuni na watu wenye kipato cha juu.

Alitahadharisha kuwa, mzigo wa kuimarisha wigo wa kukusanya mapato ya ndani usiangushwe kwa viwanda vidogo, vya kati, wajasiriamali pamoja na watu masikini pekee nchini.

“Ikizingatiwa kupanda kwa gharama za maisha na kuanguka kwa thamani ya shilingi, mshahara wenye kodi ya asilimia 30, lazima ipande kutoka Sh720,000 hadi Sh1,000,000 au zaidi na wale wa mstari wa chini lazima ipande kutoka Sh100,000 hadi Sh150,000 ili kutoa nafuu kwa watu wenye kipato cha chini,” alisema Malya na kuongeza.

No comments:

Post a Comment