Salim Said
“MIMI ni mlemavu wa kimaumbile wala si mlemavu katika kazi, lakini kuna watu ni wazima kimaumbile, lakini ni walemavu kwenye kazi,” hivi ndivyo anavyoanza Regia Mtema katika mazungumzo yake na Mwananchi.
Mtema msichana ambaye ni Afisa Mafunzo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Kurugenzi ya Organaizesheni, anasema ulemavu wake haumzuii wala kumpunguzia uwezo wake wa kufanya kazi.
Kielimu Mtema ni muhitimu wa Shahada ya kwanza katika Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua) kwenye fani ya Sayansi ya Uchumi na Lishe.
Anasema, amejipatia elimu yake ya Msingi katika shule ya msingi Mchikichini Ilala kuanzia mwaka 1989 hadi 1995, huku elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne akiipatia katika shule ya Sekondari ya Forodhani kuanzia mwaka 1996 hadi 1999 zote za jijini Dar es Salaam.
Mtema anasema, alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Benjamin Mkapa katika Mchepuo wa Kemia, Biolojia na Lishe (CBN) mwaka 2000, lakini aliomba uhamisho ili kwenda shule ya sekondari ya wasichana ya bweni Machame Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, kwa kuwa kutokana na hali yake alishachoka kusoma shule za kwenda na kurudi.
“Nilianza kuvutiwa na siasa tangu sekondari, lakini nilishindwa kujiunga na chama chochote cha siasa, kwa sababu sekondari za zamani zilikuwa hazina masuala ya siasa tofauti na sasa, ambapo matawi ya vyama yapo hata katika shule hizo,” anasema Mtema.
Anasema, akiwa Machame alivutiwa na Chadema, baada ya kutembelewa na Mwenyekiti wa sasa wa Chadema Freeman Mbowe alipokwenda kuwatembelea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2000, wakati huo akiwa ni mgombea ubunge wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro.
“Nilivutika sana na Chadema nilipokutana na Mbowe alipokuja shuleni kwetu kuomba kura mwaka 2000 akiwa ni mgombea ubunge, alinivutia sana na sera za chama chake, ingawa sikujiunga na chama kwa wakati huo, tena alishinda,” anasema Mtema.
Baada ya kuhitimu kidato cha tano na sita Mtema anasema, alijiunga na chuo cha kilimo Sua, kuanzia mwaka 2003 hadi 2006 ambapo alifanya, fani ya Sayansi ya Uchumi na Lishe na huko ndiko alikopata uamuzi wa kujiunga na siasa rasmi yani chama cha Chadema.
“Nilijiunga na Chadema nikiwa Sua mwaka 2005 kufuatia vuguvugu la kisiasa vyuoni,” anasema Mtema.
Anasema, baada ya kukamilisha masomo yake chuoni hapo, mwaka 2007 aliamua kujiunga na Chadema Makao Makuu akiwa ni Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana na Wanawake, iliyokuwa ikiongozwa na Mkurugenzi wake John Mnyika.
Anasema akiwa katika nafasi hiyo, alipata uzoefu kwa kujifunza mambo mingi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii huku akipata msaada mkubwa wa mafunzo na maelekezo ya kazi kutoka kwa Mnyika.
“Awali nilipofika makao makuu kuna wengine walidhani kama sitaweza kufanya kazi na wengine waliona nitaweza, lakini kwa ushirikiano na wenzangu nimefanikiwa sana,” anasema.
Mtema anafafanua kwamba, baada ya mabadiliko ya uongozi ndani ya kurugenzi mbalimbali za chama chao Januari mwaka huu, aliteuliwa kuwa Afisa Mafunzo katika Kurugenzi ya Oganaizesheni na Mafunzo ya Chadema.
“Hii ni sababu na ushahidi tosha kwamba kazi zangu zinakubalika kwa kuwa kama hazikubaliki nisingeteuliwa katika nafasi hii hata siku moja,” anajisifia Mtema.
Anasema, ameamua kujiunga na siasa na kuacha kazi nyingine za kuajiriwa, kwa sababu anaamini kuwa, katika siasa ni rahisi kwa mtu kutoa maoni yake na kusikilizwa pamoja na kufanyiwa kazi kwa haraka.
“Mimi ni mlemavu, lakini nyuma yangu kuna walemavu wengi, ambao hawajapata elimu kwa sababu mbalimbali zikiwamo mitazamo potofu ya jamii, juu ya watu wenye ulemavu, na kama huna elimu huwezi kuajiriwa, hivyo niliamini kuwa ipo siku moja nipata nafasi ya kuwasaidia japo kufikisha kero zao serikalini,” anasema Mtema na kusisitiza:
“Nilitaka kuja kuwasaidia wenzangu, kwa sababu kwenye siasa ndio mambo yote yanakofanyika. Utungwaji wa sera, sheria, usimamizi na marekebisho yake yanafanyika katika siasa, nilipenda na mimi niwe miongoni mwa watunga sera, sheria na hata warekebishaji.”
Akizungumzia changamoto kazini Mtema anasema, kwanza alipata ugumu kutoka katika familia yake kwa sababu hawakuwa tayari mtoto wao ajiunge na kazi ya siasa kutokana na imani waliyonayo kwamba, siasa ni fujo, vurugu na mchezo mchafu.
“Hofu yao kubwa ilikuwa ni kupoteza maadili kwa sababu wanaona siasa labda ni uhuni na ni kazi isiyo na heshma. Lakini nilitumia ujanja bila ya wao kujua,” anasema na kutoa mfano wa ujanja aliyotumia:
“Kwa mfano, baba yangu mzazi alijuwa kuwa mimi ni mwanasiasa wa Chadema Makao makuu baada ya miezi miwili, licha ya kuwa nilikuwa nalala nyumbani mwake, nakula chakula chake na nilikuwa napanda gari baadhi ya wakati kwa fedha yake, alikuwa ananiona natoka asubuhi narudi jioni, tena alijua kupitia mtu mwingine sio mimi.”
Anasema, baada ya kuja walisikitika sana, lakini ilibidi wakubali matokeo na mpaka leo hawaridhiki mimi kuwa mwanasiasa na hii inatokana na tafsiri mbaya ya siasa katika jamii kuwa ni fujo, mikiki mikiki na uovu.
Mtema anasimulia kuwa, kwa upande wa changamoto kazini, “Nilipoonekana kuwa ni mlemavu maswali yalikuja ataweza kweli? na wengine walikuwa wanaongea pembeni, na kunihukumu kuwa siwezi tu, lakini baadhi waliona naweza kina Mnyika na nimefanya nao kazi vizuri sana.”
Anasema, kwa wale walimuamini na kumkubali kuwa anaweza, wamethibitisha kwa sababu ndani ya muda wake Chadema ameweza kufanya kazi vizuri, tena wakati mwingine kuliko hata wale waliowazima na wakamilifu wa kimaumbile.
“Ulemavu wangu ni wa kimaumbile tu lakini si katika kazi,” anasema Mtema.
Anasema, baadhi ya wakati akipanda Jukwaani kabla ya kuhutubia umati wa watu katika mkutano, huwa anashangiliwa sana jambo ambalo anasema humpa maswali mingi bila ya majibu, iwapo kelele hizo ni za kukubalika kwake au la.
Mtema anasena amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kazi ya siasa hasa akiwa makao makuu ya Chadema na kwamba matarajio yake kwa sasa ni kugombania nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Baraza la Vijana la Chadema katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
“Nikifanikiwa kushinda nitakuwa nitatengeneza historia kwa sababu nitakuwa msichana na mlemavu wa kwanza Tanzania kuwa katibu mkuu wa baraza la vijana katika vyama vyote,” anasema Mtema.
Sambamba na hilo, Mtema anasema anatarajia kujitupa Jimboni kugombea ubunge katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kama Mwenyezi Mungu atamueka hai na mzima.
“Kwa mwaka 2010 ni ngumu kuingia jimboni, lakini matarajio yangu ni kuijtupa huko katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa sababu jamii bado haijawakubali ipasavyo walemavu, wanawake na vijana lakini natarajia ikifika muda huo, mwamko utakuwa wa kutosha katika jamii kuhusu sisi,” anasema.
Mbali na kuwa Afisa Mafunzo wa Chadema Mtema ni Mkurugenzi wa Vijana na Michezo katika Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata).
No comments:
Post a Comment