Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimewataka Watanzania kuupinga kwa nguvu zao zote Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF), unaotaka kuanzishwa na serikali kwa madai kuwa ni ufisadi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya alisema uanzishwaji wa mfuko huo ni ufisadi.
Alisema Watanzania wanapaswa kupinga kwa nguvu zote kuanzishwa kwa mfuko huo, kwa sababu kutokana na hali ilivyo hivi sasa utatumiwa na wanasiasa mafisadi kufanikisha malengo yao binafsi ya kisiasa na kiuchumi, badala ya kuwezesha miradi ya maendeleo kwenye majimbo.
“Watanzania wanapaswa kuupinga kwa nguvu zao zote mfuko huu, kwa sababu ni ufisadi na utatumiwa na wanasiasa mafisadi kufanikisha malengo yao binafsi ya kisiasa na kiuchumi,” alisema Nkya.
Alisema wabunge wanaoshabikia mfuko huo, uanzishwe wanafahamu kuwa utawanufaisha wao zaidi kuliko wananchi kutokana na ukweli kwamba, hakuna juhudi zilizofanyika kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kufuatilia kwa makini matumizi ya fedha zao zitakazowekwa katika mfuko huo kwa shughuli za maendeleo ya majimbo yao.
“Kama lengo la serikali kuanzisha CDF ni kuondoa umaskini majimboni, kabla hata sheria ya kuanzishwa kwake kupitishwa na Bunge, serikali ingetenga bajeti mahususi kwa ajili ya vyombo vya habari kuelimisha wananchi umuhimu wa mfuko, ushiriki wao katika kuendesha kwa ufanisi na changamoto katika usimamizi wa fedha zao,” alisema Nkya.
Alisema Tamwa wanahoji sababu za serikali kufanya haraka kupeleka muswada wa kuanzisha CDF, bungeni kabla ya kuwashirikisha wananchi katika majimbo yote ambao ndio walengwa na wadau wakuu wa mfuko huo.
Aliihoji, serikali kuwa itawahakikishiaje wananchi kwamba fedha za CDF zitatumika kwa kutekeleza vipaumbele vya wananchi na hazitaibwa na wanasiasa mafisadi, endapo fedha za umma zimewahi kuibiwa katika vyombo nyeti ikiwa ni pamoja na Sh133 bilioni zilizoibwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania(BoT).
“Ni kwa nini serikali iharakishe kupeleka muswada wa CDF bungeni bila kujiridhisha kwanza kwamba wananchi, wametayarishwa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha fedha za umma zitakazopitia katika mfuko huo zinaendesha miradi majimboni kwa viwango na kwa wakati,”alihoji Nkya.
Aliihoji serikali iwapo haioni kuwa kuwashirikisha wabunge kusimamia mfuko wa CDF, ni kudhoofisha utawala bora na hivyo kuimarisha ufisadi, ambao ni kikwazo kikubwa cha haki na maendeleo ya wanyonge nchini.
“Tamwa tunaamini kuwa Tanzania ni moja ya nchi chache duniani ambazo zimeweka utaratibu mzuri wa kuwafikia wananchi kuanzia serikali kuu, halmashauri hadi ngazi za serikali za mitaa na kwamba kinachohitajika sasa ni kuondoa umaskini majimboni na si kuanzisha mfumo mpya,” alisema Nkya.
Alisema, lengo iwe ni pia kupata viongozi wa kisiasa ikiwa ni pamoja na wabunge wenye nia ya dhati wa kusimamia serikali kuu, halmashauri na serikali za mitaa ili ziwajibike ipasavyo kwa wananchi na si kupewa fedha.
Alisema, nchi za Kenya na Sudan ambako mifuko ya CDF ilianzishwa, imekuwa ni chanzo cha kutajirisha wabunge wenyewe, ndugu zao, marafiki zao, washirika wao huku wananchi ambao ndio walengwa wa mifuko hiyo wakibaki maskini wa kutupwa.
No comments:
Post a Comment