Salim Said
SERIKALI imesema ripoti ya chanzo cha milipuko ya Mabomu iliyotokea kwenye eneo la kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam Aprili 29 mwaka huu bado haijakamilika.
Tayari miezi mitatu imetimia tangu kutokea kwa milipuko hiyo iliyosababisha mamia ya wakaazi wa eneo hilo, kuishi katika Mahema na kwa chakula cha msaada kwa muda.
Milipuko hiyo iliyolitikisa jiji la Dar es Salaam, iligharimu pia maisha ya zaidi ya watu 20 huku mamia wakijeruhiwa na kuachwa bila ya makaazi baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na milipuko hiyo.
Katika juhudi za kutafuta chanzo cha milipuko hiyo, serikali kupitia wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, iliunda Baraza Huru la uchunguzi kwa ajili ya kubaini chanzo cha milipuko hiyo iliyoacha maafa makubwa nchini.
Uamuzi huo wa kuundwa kwa baraza la uchunguzi ulitangazwa na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Emanuel Nchimbi siku chache baada ya milipuko katika mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Ngurdoto, jijini Arusha.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya Simu jana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alisema ripoti ya chanzo cha milipuko hiyo haijakamilika na kwamba wataitangaza mara tu itakapokamilika.
“Ripoti bado haijakamilika, bado inafanyiwa kazi hadi hapo itakapokamilika katika hatua zote tutaitangaza tu ikikamilika,” alisema Dk. Mwinyi.
Alipoulizwa kuwa, ni lini ripoti hiyo itakuwa tayari na kutangazwa kwa wananchi Dk. Mwinyi alijibu:
“Kwa sasa siwezi kusema siku gani itakamilika na kutangazwa kwa sababu bado inafanyiwa kazi,” alisema Dk. Mwinyi na kusisitiza:
“Wewe ukiona kimya ujue ripoti haijakamilika na ikikamilika siku yoyote ile basi tutawapatia taarifa zake.”
Aidha Dk. Mwinyi alisema, Satelati kwa ajili ya kubaini mabaki ya mabomu yaliyokuwa yamezagaa baada ya milipuko hiyo, nayo bado haijafika nchini na kwamba siku yoyote itakapofika watatoa taarifa kwa wananchi.
Siku chache baada ya milipuko hiyo baadhi ya wanaharakati na wanasiasa nchini walitoa wito wa kujiuzulu kwa Dk. Mwinyi na Naibu wake Dk Emanuel Nchimbi pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Davis Mwamunyange, kwa madai kwamba milipuko hiyo ilitokea kwa uzembe.
Hata hivyo Dk. Mwinyi aliahidi kujiuzulu iwapo baraza la uchunguzi litabaini kuwa milipuko hiyo ilitokea kwa sababu ya kukiukwa kwa taratibu za utendaji au sheria.
No comments:
Post a Comment