MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Tuesday, June 2, 2009

Rais kuhutubia Bunge la Bajeti

Salim Said
RAIS Jakaya Kikwete anatarajia kulihutubia Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza Juni 9 mwaka huu.

Katika hotuba yake, rais Kikwete anatarajia kuzaungumzia athari za mtikisiko wa kiuchumi nchini, baada ya kupokea ripoti ya timu ya wataalamu, aliyoiunda miezi mitatu iliyopita kwa ajili ya kutathmini athari za mtikisiko huo.

Tume hiyo iliyofanya kazi chini ya mwenyekiti Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Professa Benno Ndulu itawasilisha ripoti yake kwa Waziri wa Fedha na Uchumi Mustapha Mkullo Juni 4 mwaka huu.

Akitoa majumuisho ya semina ya Hali ya uchumi wa Tanzania, kwa wabunge wa Kamati ya kudumu ya Fedha na Uchumi, waziri Mkullo alisema, tume ya rais ya kutathmini athari za mtikisiko wa kiuchumi imemaliza kazi yake na itawasilisha kwake ripoti ya kazi hiyo, Juni 4 mwaka huu.

“Baada ya kwangu kuwasilisha hiyo, nitaifikisha kwa rais ambaye ataitisha kikao cha dharura cha baraza la Mawaziri ili kuijadili na hapo itakuwa ni ya serikali na si ya wizara tena,” alisema Waziri Mkullo na kuongeza:

“Kutokana na unyeti na uzito wa ripoti hiyo rais ataomba rasmi ruhusa ya kulihutubia bunge la bajeti linalotarajiwa kuanza Juni 9 mwaka huu.”

Alisema, pamoja na mambo mingine, rais anatarajiwa kuzungumzia athari za mtikisiko wa kiuchumi duniani na Tanzania kwa upekee.

“Rais ataelezea mwelekeo wa nchi kiuchumi, tuko wapi, tunaelekea wapi na serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha inainua uchumi wake baada ya kukumbwa na mtikisiko huo,” alisema Mkullo.

Alisema, athari za kiuchumi nchini ni tofauti kabisa na zile za Marekani na Ulaya, hivyo hata jina la mtikisiko huo linaweza kubadilika katika ripoti ya profesa Ndulu.

Waziri Mkullo alisema, serikali imeandaa miradi mitatu mikubwa ya kuhakikisha inaboresha bandari yake ya Dar es Salaam kwa ajili ya kukuza uchumi na pato la taifa.

“Tunao mradi wa kwanza wa kuboresha reli ya kati kutoka Isaka hadi Kigali na kutoka Isaka, Shinyanga kuja Dar es Salaam ambayo itakuwa reli ya kisasa yenye geji kubwa,” alisema Mkullo.

Alisema, mradi mwingine ni ule wa Kanda ya kusini na kaskazini (North-South Coridor) ambao utajumuisha Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, SADC na Comesa.

“Mradi wa tatu ni upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam kieneo na kina cha maji ili meli kubwa zaidi ziweze kuja kwa sababu hivi sasa mfano ukisema ushushe tani 15 milioni kwa siku unatafuta ugomvi,” alisema Mkullo.

Alisema, wafadhili wa miradi hiyo tayari wameshapatikana na wataalamu wanaendelea na kazi ya kufanya usanifu wa miradi hiyo na kwamba baada ya miezi mitatu watakutana nao.

Waziri Mkullo alisema, uundwaji wa tume ya mipango tayari umekamilika kimfumo na kwamba muda wowote kuanzia sasa rais Kikwete atatangaza timu ya wataalamu watakaoiendesha.

“Timu hii ni tofauti kabisa na ile ya mwanzo tangu enzi ya wizara ya mipango, itakuwa tume ya wataalamu na wala hamtakuwa na wanasiasa kwa sababu za kiufanisi,” alisema Mkullo.

Kwa upande wao, wabunge wingi wa kamati hiyo walioneshwa kutoridhishwa kwao na utendaji wa bandari ya Dar es Salaam na kuendelea kuwepo kwa mwekezaji wa kupakia na kupakua makontena (Tics) wakidai kuwa ni donda ndugu na serikali imeshindwa kumchukulia hatua.

No comments:

Post a Comment