MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Thursday, June 4, 2009

Mkulo: Mfumko wa bei haudhibitiki

Salim Said

SERIKALI haiwezi kudhibiti kushuka au kupanda kwa thamani ya Shilingi kwa kuwa thamani ya fedha, inategemea nguvu ya uchumi wa nchi.

Waziri wa Fedha na Uchumi Mustapha Mkulo, aliwaeleza wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi kuwa, tatizo hilo halizuiliki kwa sababu ni la kimfumo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti tutake tusitake, tatizo la kupanda na kushuka kwa sarafu ya Tanzania lipo na serikali haiwezi kulizuia kwa sababu ni la kimfumo,” alisema Mkulo.

Alifafanua, kinachofanya serikali kukabiliana na tatizo hilo ni kuangalia iwapo mzunguko wa Shilingi ya Tanzania unaendana na uchumi wa soko au vinginevyo.

“Kama mzunguko ni mbaya tunaweza kuingilia na kurekebisha lakini, kama unaendana na uchumi wa soko, hatuwezi kuingilia hata kidogo,” alisisitiza Mkulo.

Alisema, kupanda na kushuka kwa sarafu ya Tanzania kunategemea nguvu ya uchumi wa soko, mfumuko wa bei za bidhaa muhimu na upatikanaji wa fedha za kigeni kwa msimu.

“Upatikanaji wa fedha za kigeni nchini unategemea kuanza Juni hadi Disemba lakini pia tukiweza kudhibiti mfumko wa bei ya bidhaa muhimu tunaweza kudhibiti thamani ya Shilingi yetu, ” alieleza.

Kwa mujibu wa Mkulo, thamani ya Shilingi ya Tanzania imeshuka hadi kufikia wastani wa Sh1,280.30 kwa Dola ya Marekani Desemba mwaka jana ikilinganishwa na Sh1,132.09 Desemba 2007.

Alisema, mfumko wa bei kwa mwaka 2008, ulikua kwa asilimia 10.3 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2007. Kiwango cha chini cha kasi ya mfumko huo 2008, ilikuwa Januari kilipopanda kwa asilimia 8.6 na kiwango cha juu asilimia 13.5 Disemba mwaka huohuo.

“Lengo letu la mfumko lilikuwa asilimia 5.0 Juni 2008, lakini halikufikiwa kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji hasa baada ya kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta na umeme,” alisema Mkulo na kuongeza:

“Hadi April 2009, mfumko ulifikia asilimia 12.0 kutokana na hali hiyo, ambapo awali lengo la mfumko huo lilitarajiwa liwe chini ya asilimia 7.5 ifikapo Juni 2009, lakini sasa tunatarajia asilimia 11.0.”


No comments:

Post a Comment