Khamis Amani, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imepiga marufuku mambo mbali mbali yanayoenda kinyume na maadili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ikiwemo uvaaji wa nguo zisizokuwa na heshima, ili kulinda heshima ya mwezi huo.
Pamoja na marufuku hiyo, serikali imetanabahisha kuwa hatua za
kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wote watakaokiuka agizo hilo la
serikali.
Mawaziri wa wizara za Katiba na Sheria Abubakar Khamis Bakary, pamoja
na waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk,
waliyasema hayo katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani walipozungumza na
waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali.
Katika taarifa hiyo, Mawaziri hao walisema katika kipindi cha nyuma
mwezi mtukufu wa Ramadhani umekuwa ukipoteza heshima yake, kutokana na
waumini wake kuwa mstari wa mbele kuudharau mwezi huo.
“Tumezowea kuona watu wanakula ovyo, wanapiga disko mchana, uvaaji wa
nguo zisizokuwa na heshima kwa wanawake pamoja na mambo mengine, ambayo
yanaupotezea heshima mwezi huo mtukufu wa Ramadhani”, alisema waziri wa
Katiba na Sheria.
Hivyo waziri Abubakar alisema kwa kuona hayo serikali imeona ipo haja
ya kuendeleza tabia na hulka ya kuheshimu mwezi huo, kwa kupiga
marufuku mambo yote yanayokwenda kinyume na mila, silka na maadili ya
mwezi huo wa Ramadhani.
Katika marufuku hiyo, waziri Abubakar amepiga maruku kuwepo kwa
magenge ya vyakula (mama ntilie) na hoteli ndogo ndogo za kawaida kwa
mchana wote wa mwezi mtuku wa Ramadhani.
Waziri Abubakar alisema Serikali, haitoruhusu mtu yoyote wakati wa
mchana wa mwezi wa Ramadhani hata kwa yule asiyekuwa muumini wa dini ya
Kiisilamu, kuonekana akila, akinywa au akilewa hadharani, au kufanya
jambo lolote ambalo ni kinyume na maadili na silka za Zanzibar.
Pamoja na marufuku hiyo amepiga marufuku kwa mtu yoyote kwa wakati
wote kuvaa nguo zisizokuwa za heshima na zinazoonesha maumbile yake ya
siri, au nguo zinazobana ili kumfanya binaadamu mwengine kuwa na hisia
tofauti.
Sambamba na hayo, pia amepiga marufuku ‘disko toto’ kwa wakati wowote
ule, kwa madhumuni ya kuwafundisha watoto maadili mazuri ya Kizanzibari
na siyo kuiga mambo yasiyo na tija kwa vijana ambao ndio wazee na
viongozi wa taifa hili hapo baadae.
Alifahamisha kuwa, katika kipindi hicho cha sikukuu watoto wadogo
hawataruhusiwa kwenda katika sherehe baada ya saa 12 za jioni, hatua
kali za kisheria zitachukuliwa kwa mzee wa mtoto atakaekamatwa akikiuka
utaratibu huo.
“Tunaviomba vyombo vya dola na Baraza la Manispaa kuwachukulia hatua
za kisheria wale wote wanaohusika”, alisisitiza Waziri huyo wa Katiba na
Sheria.
Kwa upande wake, waziri wa Habari, Utamauni, Utalii na Michezo Said
Ali Mbarouk amesema kuwa, msimu wa utalii mwaka huu umeingia katika
mwezi mtukufu wa Ramadhani, hivyo jukumu la wadau wote
wanaujishughulisha na biashara hiyo pamoja na wananchi kwa ujumla
kuwakumbusha na kuwaelekeza wageni kujiepusha kabisa na mambo yote
ambayo hayaruhusiwi kufanywa wakati wanaofunga wakiwa katika ibada hiyo.
“Tuwakumbushe wageni wetu mambo yasiyostahiki kwa mfano kula, kunywa,
kuvuta sigara na kubusiana hadharani ni mambo ambayo hayaruhusiwi na
yanakwenda kinyume na mila, silka na maadili yetu”, alisema Waziri
Mbarouk.
Alisema kuwa hali hiyo, itasaidia kuwaepusha na matendo yoyote
yanayoweza kuleta na kusababisha waliofunga kutokubali kufanywa kwa
vitendo hivyo hadharani, na hivyo kuwa chanzo cha vurugu baina ya
waumini wa Kiisilamu na wafuasi wengine.
Alisihi kuwa, ikitokezea kwa mgeni kwenda kinyume na hayo, jamii
iepuke matumizi ya nguvu katika kurekebisha hali hiyo na badala yake
itumike busara zaidi, na kuwafahamisha wageni nini cha kufanya na maeneo
gani wanaweza kupata huduma za lazima bila ya kuvunja sheria.
Alifahamisha kuwa, kikawaida watalii ni wageni wenye uwerevu,
usikivu, utiifu na wepesi wa kufuata maelekezo ya wenyeji wao, kwa
kuzingatia hayo kila mmoja ana wajibu wa kushirikiana nao.
Alisema wizara kupitia Kamisheni ya Utalii, tayari imeshasambaza
toleo ‘circular’ maalumu katika taasisi zote zinazohusika na utalii, kwa
nia na madhumuni ya kuendeleza utalii uwe endelevu.
No comments:
Post a Comment