Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar imezifutia rasmi hati
ya kufanya kazi Meli ya Mv.Kalama, Mv.Seagul na Mv.Sepideh kutokana na
meli hizo kutokukidhi hali ya usalama wa abiria katika meli hizo.
Aidha
meli hizo zimepewa muda wa mwezi mmoja kuanzia leo kuhakikisha
zimeondoka katika maeneo ya Zanzibar kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa
dhidi ya wamiliki wa Meli hizo.
Kauli hiyo imetolewa na
Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar Abdullah Husein
Kombo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Afisini kwake
kuhusu hali ya usafiri wa baharini na usalama Zanzibar.
Amesema
Mamlaka hiyo imefanya tathmini na uhakiki wa kutosha na kujiridhisha
kuwa Meli hizo hazifai kufanya kazi katika maeneo ya Zanzibar jambo
ambalo limepelekea kuchukua hatua za kufuta hati za kufanyia kazi meli
hizo.
Amefahamisha kuwa sababu kuu zilizopelekea Mamlaka
kufanya maamuzi hayo ni pamoja na uchakavu,umri wa meli hizo kuwa mrefu
na kupata matatizo mara kwa mara katika safari zao.
Kombo amefahamisha
kuwa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri na Bandari Zanzibar ya mwaka 2006
kifungu cha 17.1 inampa mamlaka Msajili wa Meli kuifuta meli yoyote
ambayo itakuwa haikidhi usalama wa abiria.
Kufuatia sheria
hiyo Kombo amesema watawataka wamiliki wa Meli hizo kuzirudisha hati za
kufanyia kazi meli hizo ili waende kutafuta sehemu nyengine za usajili
kinyume na maeneo ya Zanzibar.
Akizungumzia Meli ya
Mv.Serengeti Kombo amesema wamelazimika kuiagiza meli hiyo kupunguza
idadi ya abiria kutoka watu 800 hadi 350 na tani za mizigo kutoka 100
hadi 50 hadi pale ambapo watajiridhisha kutokana na hali ya meli hiyo
ilivyo.
Aidha amegusia kuwa Kampuni ya Bakhresa italeta
Meli kubwa ya abiria itakayofanya kazi zake Zanzibar ambapo pia Serikali
ya Mapinduzi nayo iko mbioni kuhakikisha wanaleta meli inayokidhi
mahitaji ya wananchi wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment