Salim Said na Sadick Kaijage
SIKU moja baada ya Mufti wa Tanzania Sheikh Issa bin Shaaban Simba kusema, CCM italia kwenye uchaguzi Mkuu 2010, Mhadhir Mashuhuri wa Msikiti wa Idrissa jijini Dar es Salaam sheikh Ali Basaleh, ameitilia mkazo kauli hiyo kwa kusema, ni fatwa kutoka kwa kiongozi na itaungwa mkono na waislaam wote nchini.
Aidha, alisema kuiua mahakama ya kadhi ni ufisadi na kutoa changamoto kwa serikali kuivunja mahakama ya kadhi Zanzibar, kwa kuwa hiyo ni sehemu ya Tanzania na kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe, kuwa na mahakama ya kadhi nchini ni kuvunja katiba ya Jamhuri.
Juni 30 mwaka huu, serikali kupitia Waziri Chikawe ilitangaza kuizika rasmi hoja ya mahakama ya kadhi ambapo alipingwa vikali na Mbunge wa Kigoma Kusini, Manju Msambya (CCM), akisema kuwa haoni kosa kwa Waislamu kuundiwa mahakama hiyo.
Siku moja baadaye, Mufti Simba alizungumza na waandishi wa habari na kuwaeleza hasira za waislaam kwa kunyimwa haki yao ya kuwa na mahakama hiyo, na kuahidi hawatakipigia kura Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu 2010.
Ijumaa ya jana takriban misikiti yote jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake, hotuba za Swala ya Ijumaa ziliegemezwa zaidi katika kuwashajihisha waumini wa dini ya kiislaam kushikama kwa pamoja na kumuunga mkono mufti Simba na Msambya (mbunge) kwa ukakamavu.
Akizungumza mara baada ya Swala ya Ijumaa jana, sheikh Basaleh alisisitiza kuwa kauli ya Mufti Simba ni Fatwa isiyopingika katika jamii ya kiislaam, kwa sababu imesimama katika haki na inaendana na kauli ya Mtume Muhammad (S.A.W).
“Na sisi sote tuseme, CCM ilie tu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, sawa! Hiyo ni fatwa, aliyeitoa si Mufti? ndiyee, ni fatwa inayoendana na kauli ya Mtume Muhammad (S.A.W) imesimama kabisa,” alisema sheikh Basalehe, huku akiungwa mkono na mamia ya waumini waliojazana msikitini hapo.
Sheikh Basaleh aliongeza, ”mufti akitoa fatwa inayoendana kinyume na maneno ya Allah na kauli ya Mtume (S.A.W) tutampinga. Mtume anasema hivi, ’Muumini wa kweli haumwi na nyoka katika shimo moja mara mbili mfululizo.”
Alisema, kama kuna waislaam walioipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, 2000 na 2005 sasa imetosha na kwa pamoja waungane katika kumuunga mkono Mufti Simba kwa kutoipigia tena kura katika ngazi zote.
“Sote tumuunge mkono mufti na Msambya, tutawaunga hatuwaungi,” alihoji na kuitikiwa kwa sauti ya juu na waislaam, “tutawaungaa… haya kama tutawaunga hebu tushakane mikono na kusema kwa pamoja takbiri, ili kuonesha ishara na nia yetu ya kuwaunga,” alisema na waumini wote walishikana mikono.
Alifafanua kuwa, Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano na kwamba kuna mahakama ya kadhi, lakini Waziri Chikawe aliwambia wabunge mjini Dodoma kuwa katiba ya nchi hairuhusu kuwa na mahakama ya kadhi Tanzania.
”Mlituambia kwamba Zanzibar si nchi bali ni sehemu ya Muungano, kama hivyo ndivyo, waziri Chikawe ni Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania ’including’ Zanzibar. Ikiwa kuwa na mahakama ya kadhi bara ni kuvunja katiba, bila ya shaka na kuwa na mahakama ya kadhi zanzibar pia ni kuvunja katiba, mbona haivunjwi,” alihoji sheikh Basalehe na kutoa changamoto:
”Ivunjeni nayo, ndiyo waivunje, lakini hawawezi kwa sababu wakiivunja na muungano unazikwa hapohapo, na wajaribu tuone. Waislaam lazima tufikie wakati tuungane na kushikama kudai haki zetu na hili la mahakama ya kadhi ni muhimu sana.”
Alisema, suala la kuchanganywa kwa sheria za kiislaam na sheria za nchi haiwezekani kwa sababu ni sawa na kuchanganya chai na chumvi.
”Ndugu zangu, sheria za kiislaam ni za Allah na sheria za nchi ni za binadamu, kwa hiyo vitu hivi ni muhali kukutana ni sawa na chai kuichanganya na chumvi,” alisema.
Alisema, suala la serikali kuwanyima waislaam na kupuuza madai yao na kuyasikiliza ya makanisa ni katika mpango wake wa kuhakikisha kuwa mahakama hiyo haianzishwi ili kuwaridhisha maaskofu.
”Mbona serikali ina mahakama nyingi tu kulingana na mahitaji yake, mathalan kuna mahakama ya kazi, biashara, nyumba na kadhalika na kila mahakama kuna mahakimu wake maalumu, sasa kwa nini ishindwe kuwatendea haki waislaam,” alihoji.
Alisema, sheria za kisilamu ni ibada na hivyo hazitakiwi kutumiwa na hakimu asiyekuwa muislaam msomi wa sheria za kiislam, kwa sababu ataivuruga tu.
”Kadhi ni neno la kiarabu maana yake ni hakimu, tena hakimu bingwa, sio tuchanganye sheria ya Allah na za binadam kwa sababu tunao mahakimu, hoja si hakimu hapa hoja ni kadhi kwa maana muislaam aliyesoma sheria za kiislaam na kufaulu vizuri,” alisema.
Sheikh Basaleh alipinga kauli ya Waziri Chikawe kuwa, Afrika ya Kusini ina idadi kubwa ya waislaam na kusema kuwa nchi hiyo ina waislaam chini ya kiwango cha asilimia tano.
”Lakini hata hivyo kwa nini waziri apate tabu ya kwenda mbali kote huko? Kuna Kenya, Uganda na Zanzibar hapahapa amezipita zote anaenda kupiga mfano wa Afrika ya Kusini yenye idadi ndogo ya waislaam. Tunamwambia si kweli kuwa kuna idadi kubwa ya waislaam. Hatumwiti muongo waislaam tunma ustarabu wa kuongea,” alisistiza.
No comments:
Post a Comment