MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Thursday, July 2, 2009

Serikali imetelekeza mapendekezo ya Jaji Nyalali

Salim Said
WAKATI miaka 17 imepita tangu tume ya marehemu Jaji Francis Nyalali kutoa mapendekezo ya kuboresha demokrasia nchini mwaka 1991, wadau wa masuala ya kisiasa wamesema mapendekezo mengi ya tume hiyo hayajatekelezwa na serikali ya Tanzania.

Tume ya Jaji Nyalali iliyoundwa na rais mstaafu wa awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa madarakani mwaka 1991, ili kukusanya maoni ya watanzania kuhusu mfumo wa demokrasia nchini, ilipendekeza mambo kadhaa ya kutekelezwa kwa ajili ya kuboresha siasa za Tanzania.

Miongoni mwa mapendekezo hayo, ni pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, marekebisho ya katiba ya nchi, kuvipa meno vyombo vya bunge na baraza la wawakilishi la Zanzibar na kutoa uhuru kwa vyombo vya habari.

Mengine ni kuundwa kwa serikali tatu, kuanzishwa kwa nafasi ya mgombea binafsi, tume huru ya uchaguzi, kuwapo kwa kura uwiano, mwafaka wa kisiasa na kufutwa kwa sheria 40 nchini ambazo zilionekana kuwa zinaenda kinyume na haki za binadamu na utawala bora.

Wadau hao walisema hayo jana katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) Ubungo jijini Dar es Salaam, kujadili mafanikio ya utekelezwaji wa mapendekezo ya tume hiyo katika kuboresha demokrasia nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba alisema, kati ya mambo mengi yaliyopendekezwa na tume huru ya Jaji Nyalali ni pendekezo moja tu la kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ndilo lililotekelezwa kikamilifu, huku mengine yakiishia hewani.

“Tumefanikiwa jambo moja tu la kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa huku mengine yakiishia hewani, ndio mana tunatawaliwa na vurugu kubwa katika chaguzi zote zinazofanyika nchini mara kwa mara,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema, kitendo cha serikali ya Tanzania kuyatelekeza mapendekezo mengi ya tume ya marehemu jaji Nyalali, demokrasia ya Tanzania haikui kutokana na vyombo vingi vya demokrasia kukitumikia Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Swa tumeanzisha mfumo wa vyama vingi, lakini yale mambo yaliyopendekezwa kwa ajili ya kurutubisha na kuimarisha mfumo huo tumeyaacha, jambo hili litatuletea matatizo makubwa katika chaguzi zijazo iwapo hayatatekelezwa,” alisema profesa Lipumba.

Alisema, tume za uchaguzi, katiba ya nchi na sheria za nchi zilizopo si za kidemokrasia kwa kuwa, zitatumikia zaidi Chama tawala CCM badala ya kutumikia wananchi wote na demokrasia ya nchi.

Alifafanua, tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza kufutwa kwa sheria 40 nchini, ambazo zilionekana kuwa zinakandamiza haki za binadamu, lakini sheria hizo hadi sasa zinaendelea kutumika, huku serikali ikiongeza sheria nyingine za ukandamizaji.

“Tutayajadili kwa undani mambo haya, ili kuona ni kwa kiwango gani tumefanikiwa au kufeli, lakini kiufupi hatujafanikiwa kwani zile sheria 40 hazijafutwa na nyengine zimeongezwa ikiwamo ya ugaidi,” alisema profesa Lipumba.

Kwa upande wake mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Nape Nnauye aliitaka serikali kuhakikisha inayachukua na kuyafanyia kazi mawazo ya wadau, ili kuboresha demokrasia ya Tanzania.

Alikiri kuwepo kwa upungufu mwingi katika utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya Jaji Nyalali, lakini kwa kiasi fulani alisema serikali imejitahidi na kufanikiwa kuboresha demokrasia ya nchi.

“Ni kweli kuna upungufu katika utekelezaji wa mapendekezo ya jaji Nyalali, lakini pia lazima tukiri kuwa serikali kwa upande wake imejitahidi na yapo mafanikio makubwa tumepata katika demokrasia ya nchi yetu. Ila ni vyema serikali ikayaangalia mawazo ya wadau katika semina kama hizi na kuyafanyia kazi kuliko kuyaacha yakiishia hewani,” alisema Nnauye na kuongeza:

“Katika semina hii wadau watajadili tulikotoka kisiasa na kidemokrasia, tupo wapi na tunaelekea wapi, ili tuweze kujirekebisha pale tulipokosea na kujiimarisha tulipopatia.”

Naye Waziri wa Katiba na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Ramadhan Shaban alisema, nchi inakabiliwa na changamoto nyingi katika kuboresha demokrasia.

“Kwanza tunakabiliwa na changamoto ya kuondoa hofu ya wananchi kutoa maoni yao katika tume huru, kuzingatia amani na utulivu katika kufanya kazi za kisiasa na kuhakikisha kuwa vyombo vinavyohusika na utungaji wa sheria na kurekebisha katiba vinawapatia watanzania, sheria na katiba zinazokidhi haja na matakwa yao,” alisema Waziri Shaban na kuongeza:

“Pia tunapaswa kuhakikisha kuwa watendaji wetu wa serikali hawajishughulishi na shughuli za kisiasa, ili kuepusha migongano mikubwa ndani ya serikali na hivyo kuanguka kwa ufanisi wake katika kuwatumikia wananchi, kama chachu ya kuleta maendeleo.”

No comments:

Post a Comment