MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Sunday, January 16, 2011

Waislaam wachoshwa na Mfumo Kristo kuongoza nchi

Waitaka serikali kusema kama
imeshindwa, ili wachukue hatua
Salim Said
WAISLAAM Tanzania wametoa tamko lao kuhusu kauli mbalimbali za maaskofu na vurugu za Arusha zilizosababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi 29 huku wakionya kuwa, dhuluma ya udini italisambaratisha taifa miaka michache ijayo iwapo Serikali haitachukua juhudi za makusudi kudhibiti hali hiyo iliyojitokeza kwa kasi nchini.

Katika tamko hilo pia Waislaam wamewatuhumu maaskofu nchini kwamba ndio waliochochea vurugu hizo kwa lengo la kuingia madarakani kwa nguvu, baada ya Chama, ilani na Mgombea wao kukataliwa na Watanzania katika Uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 mwaka jana.

Tamko hilo linaonyesha mpasuko wa wazi baina ya viongozi wa dini wa kiislaam na wa kikristo kuhusu mgogoro na vurugu za Arusha.

Akisoma Tamko hilo kwa niaba ya Waislaam nchini, Mhadhiri Mashuhuri wa Msikiti wa Idriisa Jijini Dar es Salaam, Sheikh Ali Baswaleh (Mzee wa Kunukuu), aliitaka serikali na chama tawala kuwaeleza Watanzania kama imeshindwa kusimamia haki, ili waislaam wachukue hatua ya kulinda haki zao kwa gharama yoyote ile.

“Madam mfumo kristo umeimarika kiasi kiasi cha kuitisha serikali na viongozi wake na wakatishika hadi kuomba radhi, na kuvitisha na hata kuvikemea vyombo vya dola na kusalimu amri, waislaam tukatae,” alisema Sheikh Baswaleh na kuongeza:

“Kama alivyotahadharisha Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ukweli ni kwamba hatupita muda mrefu dhuluma ya udini utalisambaratisha taifa letu kama ulivyolisambaratisha la Ivory Coast ambalo miaka ya 1960 na 1970 lilkuwa mfano wa kuigwa duniani.”

Huku akiungwa mkono na kutiwa hamasa na takbiri kutoka kwa maelfu ya waislaam walifurika katika ukumbi wa Diamond Jublee, Sheikh Baswaleh alisisitiza, “Kwa kuwa tunadhalilishwa na kubaguliwa kwa sababu ya uislaam wetu nchini mwetu, hatuna budi kushikamana kama waislaam.”

Sheikh Baswaleh alisema dhuluma ya udini haitaondolewa na Katiba Mpya hivyo ni wajibu wa kila muslaam kupigania ukombozi kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa katiba mpya wakiwa raia huru sawa na wenzao.

“Waislaam popote tulipo tunao wajibu wa kuorodhesha dhuluma za udini tunazofanyiwa na kupigania ziondolewe kwanza na baadaye kulipwa fidia,” alisema Baswalehe.

Baswaleh alitaja baadhi ya mifano ya dhuluma hizo za udini kuwa ni Sheria ya Ugaidi, Mkataba baina ya Serikarli na Kanisa (MoU), Mauaji ya Mwembe Chai, Maandamano ya Dibagula, mauaji ya Waslaam Zanzibar, Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwaomba radhi maaskofu Sumbawanga, Samuell Malecela kumtaka aliyewaambia maaskofu wa Arusha wavue majoho ya dini na wavae ya siasa awaombe radhi.

Alisema katiba mpya haiwezi kulinda haki za madhalimu na wadhulumiwa kwa wakati moja na ingawa kipropaganda Tanzania ni nchi moja lakini kuhalisia ni nchi yenye jamii mbili zenye hadhi tofauti.

“Umefika wakati sasa wa kuigawana nchi ili waislaam wanaonyanyaswa na kudhulumiwa waishi katika maeneo yenye waislaam wengi na wakristo wanaotukuzwa waishi katika maeneo ya wakristo wengi, kama Mwalimu Nyerere Julius alivyotetea na kusaidia kujitenga kwa Biafra nchini Nigeria kutokana na udini,” alisema Baswaleh.

Sheikh Baswaleh alisema, “Tukifanya hivyo waislaam watapata uhuru wa kujiamulia mambo yao kama ya mahakama ya kadhi na kujiunga na kongamano la jumuiya za kiislaam duniani (OIC) na sio kuamuliwa na maaskofu.”

Alisema ni wajibu wa kulifikisha hilo kwa waislaam wote nchini ili lijadiliwe kabla halijafikishwa rasmi serikalini kama mapendekezo ya waislaam katika mchakato wa kuunda katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tamko hilo lenye anuani ya ‘Tamko la Waislaam dhidi ya Maaskofu’ na kurasa 13 liliibua hamasa kwa waislaam huku Takbiir na Innnaa Lillaahi zikitawala kuonyesha kuunga mkono au kusikitika katika baadhi ya aya, lilimnukuu nyerere katika kitabu chake kwamba anayedhulumiwa ni mtu anayeteseka na kwamba asipopambana ataendelea kuteseka na dhalimu kuendelea kunufaika.

“Umefika wakati sasa wa kugawana machungu ya udini tuliyoyabeba peke yetu waislaam kwa miaka 50 ya uhuru Tanzania,” alisema Sheikh Baswaleh huku akiungwa mkono kwa takbiir…Allahu Akbar.

Tamko hilo lilikuwa na sehemu za utangulizi, hali ya siasa nchini, maazimio na dalili ya mvua ni mawingu lilisikilizwa na maelfu ya waislaam waliohudhuria hapo kutoka nchini kote na kusikilizwa moja kwa moja kupitia Redio Iman ya Morogoro na Redio nyingine za kiislaam Dar es Salaam.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Baraza Kuu la Waislaam Tanzania (Bakwata), Alhad Mussa Salum ambaye alikuwapo katika hafla hiyo, aliunga mkono tamko hilo na kusisitiza kuwa litaleta heshima kwa waislaam.

“Tamko ni zuri na naamini litaleta heshima kwa waislaam cha msingi ni vyema serikali na wakristo wakawajali na kuwaheshimu waislaam kama raia halali wa Tanzania katika haki zao,” alisema Sheikh Salum.

Awali mwakilishi wa waislaam wa Mwanza Sheikh Kapungu Ilunga aliwatuhumu vikali maaskofu kuwa ndio chanzo cha vurugu za Arusha.

“Maaskofu walipoona ilani yao, Chama chao cha Chadema, mgombea wao Padri mwenzao Dk Willibrod Slaa amekataliwa na watanzania wakaamua kuchochea vurugu kwa lengo la kutaka kuingia madarakani kwa nguvu zote,” alisema Ustadh Ilunga huku akishangiriwa.

“Lakini, ‘who are’ maaskofu katika serikali na nchi hii? Ni nani hasa maaskofu mpaka serikali iwapigie magoti, ishindwe kuwakemea, kuwaonya na mwenendo wao,” alihoji Ilunga huku akijibiwa na umma wa Waislaam kuwa, si chochoteee…taka taka tu.

“Tunawaweza sisi maaskofu, tunaweza kuwanyamazisha maaskofu, tunachotaka kama serikali imeshindwa kuwawajibikia watanzania walioiweka madarakani iseme ili waislaam tulinde haki zetu kwa gharama yoyote,” aliongeza Ilunga alipokuwa akiwasilisha mada ya ‘Uislaam na Hatari ya Mfumo Kristo Tanzania’.

Naye Sheikh Ponda Issa Ponda alisema kuna haki za kikatiba za watanzania ambazo serikali na polisi wanapaswa kuzilinda na kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeachiwa kuzikiuka au kuziminya.

Mkutano huo wa aina yake ulihudhuriwa na Taasisi na Jumuiya zote za kiislaam nchini ikiwa ni pamoja na Bakwata, Baraza Kuu na Jumuiya za Kiislaam (T), Islamic Propagation Center (IPC), Chuo Kikuu cha Waislaam Morogoro (MUM), Taasisi ya Wasomi wa Kiislaam (Tampro) na Taasisi ya Answari Sunna na nyingine nyingi kutoka kila kona ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment