*MWENYEWE ADAI KUTUMWA NA MFANYABIASHARA MASHUHURI JIJINI DAR ES SALAAM
Salim Said
KATIKA hali isiyo ya kawaida mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Athuman Said (53) amekamatwa akifukia vitu vinavyosadikiwa kuwa vya kishirikina huku akiwa na silaha za jadi katika nyumba ya Mkazi wa Kiluvya Gogoni Jijini Dar es Salaam, Shamsa Salum na kudai ametumwa na mfanyabiashara mashuhuri Abdallah Maliki.
Uchunguzi wa Mwandishi umebaini kuwa, Maliki ni mmiliki wa kampuni ya maji safi ya Cool Blue na Matofali ya Tembo zote za jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo la aina yake lilitokea juzi saa 4:00 usiku, baada ya mtu huyo aliyedai kuwa ni mkazi wa Kigamboni jijini hapa, kuamua kufunga safari hiyo hadi Kiluvya kutekeleza kazi ya mfanyabiashara huyo ambaye Mwandishi amebaini kuwa ni shemeji wa Shamsa.
Kwa mujibu wa mtu huyo aliyekuwa amevaa bagalashia alidai kuwa alitumwa na Maliki kwa ajili ya kwenda kuomba dua katika eneo hilo ili kumaliza mgogoro katika yake shemeji yake (Shamsa) uliodumu kwa miaka kadhaa.
Said alimwambia mwandishi wa habari hili katika eneo la tukio kuwa, yeye ni mfanyabiashara wa magari kati ya Tanzania na Arabuni, lakini pia huwa anafanya shughuli hizo za kuombea watu dua.
Mtu huyo alikuwa na tasbihi, kitabu chenye maandishi ya lugha ya kiarabu, herizi ambayo alidai kuwa ina ngozi ya kondoo ndani yake na silaha ya jadi aina ya panga, kwa ajili ya kuchimbia chini ya mlango wa nyumba hiyo ili kufukia herizi hiyo.
“Mimi nimeletwa kwa gari na mfanyabiashara huyo hadi hapo kituo cha Gogoni na kuniacha ili nije kumfanyia kazi yake, mimi na Maliki ni marafiki wa muda mrefu,” alisema Said.
Alisema lengo kuu la yeye kwenda hapo lilikuwa ni kumuomba Mungu ili kasi au kumaliza kabisa mgogoro kati ya mfanyabiashara huyo na shemeji yake Shamsa.
Mwandishi alibaini kuwa, kwa miaka kadhaa mfanyabiashara huyo na Shamsa wana mgogoro wa kugombania mali za urithi, baada ya mume wa Shamsa ambaye ni ndugu na mfanyabiashara huyo kufariki dunia.
Utafiti umebaini kuwa mfanyabiashara huyo alishafanya majaribio kadhaa ya kumtoa kwa nguvu Shamsa katika nyumba na eneo ambalo alikuwa akiishi na marehemu mumewe, ambalo analishikilia hadi sasa.
Baaadhi ya majaribio hayo ni pamoja na kutumia vikao vya familia, kwenda mahakamani, kutoa vitisho na kutumia kampuni za udalali kwenda kumtoa kwa nguvu mwanamke huyo katika nyumba.
Lakini majaribio hayo yalishindwa baada ya Mahakama ya Nyumba Wilaya ya Kinondoni kuhukumu Shamsa arudishwe katika nyumba hiyo siku mbili tu baada ya kuhamishwa kwa nguvu na shemeji yake huyo.
Hata hivyo kijana huyo alifikishwa katika kituo Kidogo cha polisi Kiluvya Gogoni saa 5:00 usiku na baadaye kuhamishiwa kituo cha polisi cha Mbezi, ambapo siku yapili alitoka kwa dhamana ya watoto wake.
Wakati huo huo Shamsa alijeruhiwa kwa panga katika mkono wake wakati wa purukushani za kumkamata mtu huyo anayesadikiwa ni mganga wa kienyeji aliyedai kutumwa na mfanyabiashara huyo kusuluhisha mgogoro kwa njia hizo.
Shamsa alidai kuwa, mfanyabiashara huyo ana njama za kumdhuru na kutaka kumuua na kwamba hana amani katika maisha yake kwa kuwa shemeji yake huyo amekuwa akifanya majaribio mbalimbali ya kumdhuru na hilo la kumtuma mganga wa kienyeji ni moja kati ya hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Elias Kalinga alisema hajapata taarifa ya tukio hilo kwa kuwa yeye huzungumzia taarifa za matukio yanayokuwa katika rekodi na kufikishwa mezani kwake.
“Lakini ngoja nitafutilia tukio hilo, nipigie muda mwengine labda nitakuwa nimepata taarifa zake,”aliahidi Kalinga.
Baada ya kupata taarifa za kunasuka kwa jaribio hilo na kwamba taarifa ziko kwa waandishi wa gazeti hili, siku ya pili Mfanyabiashara huyo alimtumia shemeji yake (jina linahifadhiwa) kumtafuta mwandishi ili kuiua habari hiyo kwa madai kuwa, kama itachapishwa itamchafulia jina lake kwa kuwa yeye ni mtu mashuhuri jijini hapa.
“Mimi nimetumwa na (mfanyabiashara huyo) yupo nje ya nchi, lakini tunawasiliana kwa simu nimeomba namba yako kwa mtu mmoja ndio nikapata,” alisema na kuongeza:
“Uhusiano wetu mimi na mfanyabiashara huyo ni kwamba, yeye ana kaka yake baba na mama mmoja anaitwa Salum Mwanamboka ambaye amemuoa dada yangu, kwa hiyo mfanyabiashara huyo ni kama shemeji yangu.”
Hata hivyo mtu huyo kabla ya kukutana na Mwandishi wa habari hii alituma ujumbe mfupi wa maneno uliosomeka, “Kuna ‘issue’ ya huyo mama (Shamsa) juzi aliwachukua waandishi kutoka huko kwa ajili ya kumdhalilisha shemeji yake (mfanyabiashara huyo), ambaye wana ugomvi mahakamani. Tafadhali izuiye.”
Juhudi za kumpata Maliki kujibu tuhuma hizo hazikufanikiwa kwa kuwa simu zake zote za mkononi hazipatikani kila alipopigiwa.
No comments:
Post a Comment