MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, February 24, 2010

ZEC yaanzisha zoezi maalum kutambua waliokuwa hawajaandikishwa

Salim Said
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) imeanzisha kazi maalum ya kuorodhesha na kutambua idadi kamili ya wazanzibari waliokosa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa sababu ya Kitambulisho cha Mzanzibari Mkazi (Zan ID) ili kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo.

Kazi hiyo inafanyika kwa siku sita tu katika mikoa na wilaya zote za Unguja na Pemba kabla ya kuanza kwa awamu ya pili nay a mwisho ya uboreshaji wa daftari hilo, inayotarajiwa kuanza Machi 1 mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa Zec Salim Kassim alisema kazi hiyo imeanza tangu Febuari 22 mwaka huu na itakamilika Febuari 28.

“Tumeamua kufanya hivi kwa sababu kumekua na malalamiko mengi kutoka kwa vyama vya siasa kwamba watu wao wengi hawajaandikishwa, tukiwauliza wangapi wanasema wengi lakini hawana idadi kamili,” alisema Kassim na kuongeza:

“Kwa hiyo kazi hii ya siku sita itatupatia orodha ya idadi kamili ya watu waliokuwa hawajaandikishwa, ili tuone kwamba ni kwa namna gani wanaweza kupata haki yao kama wana sifa, kwa sababu hawa ni wapigakura wetu.”

Alisema baada ya kukamilika kwa kazi hiyo hapo Febuari 28 hatua ya kwanza watakayochukua ni kutangaza idadi kamili ya watu hao, na baadae hatua nyengine zitafuata za kiutendaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano na Umma wa CUF Salim Bimani aliwataka wananchi wote wa Zanzibar, ambao mwaka 2005 walipiga kura katika uchaguzi mkuu na wanazo shahada zao za kupigia kura, lakini hawana Zan ID, wafike kwenye vituo vya Tume ZEC kwa wingi.

Alivitaja vituo kuwa kwa Unguja ni pamoja na Kariakoo wilaya ya Mjini, Kwerekwe ‘A’ wilaya ya Magharibi, Koani Banda la Karafuu wilaya ya Kati, Ofisi ya Wilaya Dembra wilaya ya Kusini, Gamba Banda la Karafuu wilaya ya Kaskazini ‘A’ na Mahonda Banda la Karafuu wilaya ya Kaskazini ‘B.

Kwa upande wa Kanda ya Pemba aliwataka wafike Skuli ya Micheweni wilaya ya Micheweni, Kilimo Weni wilaya ya Wete, Mtambile Banda la Karafuu wilaya ya Mkoani na kwa wilaya ya Chake Chake Wafike Skuli ya Michakaini.

Bimani aliwahimiza wananchi wote wenye sifa hizo wajitokeze kwa wingi kwenye vituo hivyo, wakizingatia kwamba kuandikishwa ndiko kutakowawezesha kupiga kura na hivyo kuwa na nguvu ya kufanya mabadiliko katika nchi yao.

“Baada ya kutambuliwa wote waliokuwa hawajaandikishwa Zec itabidi isimami kazi ya kupata Zan ID ili na wao waandikishwe katika daftari na waweze kutumia haki yao ya msingi ya kupigakura ya maoni na katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu,” alisema Bimani.

No comments:

Post a Comment