Salim Said na Kizitto Noya
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha amewajia juu vigogo wenzake serikalini kwa kumzuia kusimamia ipasavyo kazi ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa inayotarajiwa kugharimu kiasi cha Sh200 bilioni.
Akitoa majumuisho ya bajeti ya wizara yake bungeni mjini Dodoma jana, Waziri Masha alisema baadhi ya vigogo walimzuia kuhoji dosari aliyoiona katika mchakato wa zabuni ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa, wakati yeye ndiye waziri mwenye dhamana na wizara hiyo.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Waziri Masha alidaiwa kumwandikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa kuna kigogo mmoja Ikulu (jina tunalihifadhi) alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupeleka taarifa ya utekelezaji wa mradi wa vitambulisho kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri.
Ilidaiwa katika malalamiko ya Masha kwa Waziri Mkuu kuwa hatua hiyo ya kigogo huyo wa Ikulu haikumridhisha (Masha) kwa madai kwamba, hakumhusisha kwa vile yeye ndiye atakayeiwasilisha taarifa hiyo kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri na ndiye atakayewajibika kwa maamuzi yoyote yatakayofanyika wizarani kwake, bila kujali kama maamuzi hayo yalipata baraka (ya kigogo huyo) au la.
Kwa mujibu wa habari ambazo ziliandikwa na vyombo vya habari na kuthibitisha na Waziri Mkuu wakati akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni, alikiri kupokea barua ya Waziri Masha, lakini habari hizo zilivuja baada ya nyaraka kunyofolewa katika Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Masha alimwandikia Waziri Mkuu barua akimlalamikia kwa madai ya kigogo huyo kumwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani kuwasilisha taarifa hiyo kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri bila kumhusisha yeye kama Waziri.
Akiongea bungeni jana, Waziri Masha alisema wabunge wengi wamehoji mradi wa vitambulisho katika hoja tatu ambazo ni kwa nini vinachelewa, kwa nini waziri aliingilia na kwa nini halijapelekwa katika Baraza la Mawaziri.
“Mheshimiwa Naibu Spika, mheshimiwa Anna Komu ameuliza swali zuri hapa kwamba katika mradi wa vitambulisho kuna nini? Na mimi nauliza katika mradi wa vitambulisho kuna nini,” alihoji Masha.
Akizungumza huku akikariri mara kwa mara swali la kuna nini katika mradi wa vitambulisho, Waziri Masha alisema, kuna baadhi ya wabunge walimuona kafanya makosa yeye kumuhoji Katibu Mkuu na kumuandikia Waziri Mkuu kumuelezea dosari aliyoiona katika mchakato.
“Mradi upo katika mchakato, lakini baadhi ya watu hawaridhiki. Mimi niliuliza swali kwa katibu mkuu wangu, nikaambiwa nimeingilia mchakato na sina haki ya kuuliza, lakini bunge lina haki ya kunihoji mimi. Nami nauliza katika mradi huu kuna nini,” alihoji na kuongeza.
“Cha ajabu ni kwamba, mimi niliuliza ili nitakapokuja ulizwa bungeni niweze kujibu, lakini kumuuliza kwangu ilikuwa ni kosa, naambiwa hukutakiwa kuuliza. Kwa nini Bunge liniulize mimi halafu mimi nisiwe na haki ya kuuliza watendaji wangu. Hivi ndani ya mradi wa vitambulisho kuna nini?”
Waziri Masha alihoji zaidi kuwa kuna nini Watanzania na baadhi ya wabunge wasiipe muda serikali kukamilisha mradi huo, badala yake wanamtaka waziri mwenye dhamana asihoji wala kuingilia mchakato wake.
Alifafanua kuwa cha ajabu ni kwamba, kuna hoja inayotaka hata Rais na Baraza la Mawaziri hawatakiwi kupewa taarifa, huku ikisema kuwa Bunge linapaswa kujua.
“Cha ajabu kuna hoja bungeni kwamba, hata rais na baraza lake la mawaziri hawapaswi kupata taarifa za mchakato huu, lakini Bunge linapaswa kupewa taarifa, hivi kuna nini kwenye mradi huu,” alihoji Waziri Masha.
Alisema suala la mradi wa vitambulisho lipo katika mchakato na kwamba, anawaomba wabunge wampe muda kukamilisha mchakato wa zabuni ya mradi huo.
“Tumeshapokea taarifa ya PPRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi), sasa tunasubiri taarifa ya Mwanasheria Mkuu wa serikali ili suala hilo lifikishwe kwa Baraza la Mawaziri. Napenda kuona kabla ya kumalizika kwa Bunge huu mradi unaanza,” alisema.
Awali Waziri Masha alilalamika kuwa asibebeshwe lawama kwa kuchelewa vitambulisho hivyo kwa kuwa suala hilo lilianza kabla hajazaliwa mwaka 1968 huku mama yake akiwa na umri wa miaka 19 tu.
Alisema, sheria ya vitambulisho hivyo ilitungwa mwaka 1986 na mwaka 1995 tenda ya kwanza ikatangazwa ambayo hata hivyo haikufanikiwa.
Alisema, mnamo mwaka 2004 upembuzi yakinifu ulifanyika na Febuari mwaka 2007 ikakubali ushauri na kuiteua kampuni ya Gotham kuwa mshauri mwelekezi wa mradi huo.
“Hapo ndipo Masha alipofahamu mradi wa vitambulisho. Kwa hiyo hata mimi nauliza kuna nini ndani ya mradi huu,” alilalamika Masha.
Alisema hadi sasa mamlaka ya kusimamia na kuratibu utoaji wa vitambulisho hivyo (NIDA) imezinduliwa, watendaji watajiriwa na kamati ya uongozi kuteuliwa na kasha kuanza kazi.
“Pia wizara imekamilisha hatua ya kwanza ya kumpata mkandarasi ambaye ataweka mfumo wa kutunza taarifa za watu watakaopewa vitambulisho,” alisema.
Kwa mujibu wa Masha, miradi hiyo inaenda sambamba na maandalizi ya utoaji zabuni ya vitambulisho hivyo yanayoendelea sasa.
“Naomba kuwathibitishia Watanzania kupitia Bunge lako tukufu kwamba, mradi wa vitambulisho utakamilika kwa kufuata sheria na utaratibu, bila mizengwe, kwa uwazi unaostahili na bila upendeleo,”alisisitiza.
Baada ya Waziri Masha kumaliza kutoa hoja alisimama mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, (CCM) na kusema kwa jazba kuwa wanachokitaka kwa Waziri ni lini vitambulisho hivyo vitapatikana.
“Kama waziri mwenyewe hajui kinachoendelea katika wizara yake ina maana hakuna kinachoendelea, halafu anatuambia mchakato unaendelea, mchakato gani huo,” alihoji Shelukindo.
Masha alijibu, kwa kusema, “Mheshimiwa Naibu Spika narudia tena kuhoji katika mradi wa vitambulisho kuna nini? Waraka wa Baraza la Mawaziri ni siri.”
“Kuna nini katika mradi wa vitambulisho kinachawanfanya baadhi ya wabunge wasitake sisi kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali? Nauliza tena kuna nini,” alihoji Waziri Masha kwa sauti ya chini kabisa.
Alisema, Masha ni yule yule hajabadilika, amaamini kuwa anaweza, lakini na aliuliza tena kuna nini katika mradi wa vitambulisho.
Jambo hili lilisababisha Naibu Spika Anne Makinda kusimama na kutoa ufafanuzi akisema: “Mheshimiwa waziri na mheshimiwa mbunge hapa tunasikilizwa na wananchi nchi nzima, wanachotaka kujua ni je, vitambulisho watavipata au hawatavipata? Hilo ndilo wanalohitaji na sio kuna nini”.
Waziri Masha baada ya hapo alisimama na kujibu kwa ufupi kuwa, vitambulisho hivyo vitapatikana ndani ya mwaka huu wa fedha.
“Mheshimiwa Naibu Spika, vitambulisho vitapatikana ndani ya mwaka huu wa fedha,” aliahidi.
Hata hivyo, kambi ya upinzani ilieleza wasiwasi kuhusu kukamilika kwa mradi huo, ikisema serikali imekuwa ikiahidi bila kutekeleza.
Msemaji wa kambi hiyo katika wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ibrahin Muhammed Sanya alisema serikali imekuwa ikitoa ahadi zisizotekelezeka kuhusu suala la uraia wa nchi mbili na vitambulisho vya Uraia.
“Katika hotuba zetu za kambi miaka 2006/2007, 2007/2008 na 2008/2009, tumekuwa tukizungumzia suala la uraia wa nchi mbili, Na katika majibu ya Serikali mara zote ni kwamba mchakato unaendelea huku muda ukiyoyoma. Je, mchakato huo utamalizika lini? alihoji Sanya.
Akinukuu majibu ya serikali ya mwaka 2006 kuhusu vitambulisho vya uraia, Sanya alihoji: “Toka mwaka huo hadi sasa 2009, bado mchakato unaendelea tu. Kila siku tunaambiwa hadithi mpya kuhusiana na vitambulisho hivyo. Fedha za walipakodi zinazidi kuwaneemesha baadhi ya watu katika kadhia nzima ya vitambulisho vya uraia. Je Serikali inawatendea haki Watanzania?”
No comments:
Post a Comment