Salim Said
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Mwinyi amekiri kuwa, atajiuzulu iwapo Baraza la Uchunguzi wa chanzo cha milipuko ya mabomu katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mbagala jijini Dar es Salaam, Aprili 29 mwaka huu, litagundua kuwa milipuko hiyo ilitokea kwa uzembe au ukiukwaji wa taratibu na kanuni za mfumo utendaji.
Hata hivyo Dk. Mwinyi alishusha tuhuma kwa mamlaka zinazoshughulikia ugawaji wa viwanja nchini kwa kugawa viwanja hadi karibu na maeneo ya kambi za JWTZ nchini.
Milipuko ya mabomu Mbagala iligharimu maisha ya watu karibu 30, kujeruhi mamia na kuharibu makazi ya maelfu ya watu na nyumba kadhaa za Ibada ikiwamo misikiti na makanisa.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) kwenye kipindi chake cha ‘Jambo Tanzania’.
“Ikibainika kuwa kuna uzembe wowote wa kimfumo au kiutendaji uliosababisha kutokea kwa milipuko ya mabomu ya Mbagala, Waziri atawajibika,” alisema Dk, Mwinyi na kusisitiza:
“Milipuko ile ilikuwa ajali na wala si uzembe kwa sababu kabla ya Braza la uchunguzi kuanza kazi yake, tulishaangalia majengo yalikuwa mazima kabla ya milipuko, ukaguzi wa mabomu ulikwishafanyika na hata milipuko ilipotokea mlikuwa na watu watano.”
Awali Dk. Mwinyi alikuwa mgumu kukiri utayari wake wa kujiuzulu akisisitiza kuwa milipuko hiyo, ilikuwa ni ajali na kwamba kiongozi hapaswi kujiuzulu kwa matukio ya ajali, bali hujiuzulu kwa uzembe au ukiukwaji wa sheria, taratibu au kanuni za kiutendaji.
“Mimi naamini ile ilikuwa ajali ya kawaida na hakuna uzembe wala ukiukwaji wa taratibu, na kwa maana hiyo waziri hapaswi kujiuzulu kwa matukio ya ajali, kwa sababu kama ni hivyo ajali kila siku zinatokea na hakuna anayejiuzulu kutokana na ukweli kwamba ni vigumu kuzuia ajali,” alisema Dk. Mwinyi.
Alikiri kupata shinikizo la kujiuzulu, lakini alibeza na kusema shinikizo hilo linatoka kwa wanasiasa wa upinzani, ambao wanataka kufanya siasa hata katika sehemu na wakati wa majanga.
Aidha Dk. Minyi alisema, watu wote watano waliokuwamo katika ghala hilo la mabomu, walipoteza maisha na kwamba kuna watu wawili waliokuwapo nje akiwamo mwanajeshi mmoaja na raia mmoja, ambao watatumika kama hadidu za rejea.
Alisema, baraza la uchunguzi lililoundwa ni zuri na kwamba litatoka na chanzo sahihi cha milipuko hiyo na mapendekezo ya kujilinda ili tatizo kama hilo lisitokee tena nchini.
Kuhusu kuendelea au kutoendelea kwa makazi ya watu karibu na kambi za JWTZ dk, Mwinyi alisema, “kwa sababu tatizo kwa sasa lipo katika kambi ya Mbagala na kuna nyumba zilizobomoka, mategemeo ni kutowarudisha tena waliobolewa nyumba zao na tutaangalia mapendekezo ya kamati kuhusu ‘buffer zone’ umbali kutoka kambini na makazi ya watu, halafu tutafanya nchi nzima.”
Hata hivyo Dk. Mwinyi alikataa kutaja tarehe ya mwisho waliyopewa baraza la uchunguzi akisisitiza kuwa, “kwa sababu ni kazi ya kitaalamu tunapaswa kuwapa muda wa kutosha bila ya kuwabana, ili watoke na ripoti nzuri, lakini tuliwapa maelekezo tu kabla ya kuanza kazi kwamba, wafanye kazi haraka iwezekanavyo.”
Aidha Dk Mwinyi alisema, uvamizi wa watu katika makambi ya JWTZ ni kutokana na utendaji wa mamlaka zinashoghulikia ardhi nchini, ambapo alizitaja serikali za halamashauri na wizara ya ardhi.
Miongoni mwa athari za milipuko ya Mbagala ni tisho la baadhi ya watu kupata ulemavu wa kusikia na kuona ambapo hadi sasa zaidi ya watu 1600 wameripotiwa kuwa na matatizo hayo.
No comments:
Post a Comment